“Kavazi (2014 – 2019): Jukwaa la kujifunzia, udadisi na mijadala”

“Kavazi (2014 – 2019): Jukwaa la kujifunzia, udadisi na mijadala”

“Kavazi (2014 – 2019): Jukwaa la kujifunzia, udadisi na mijadala”

Kavazi la Mwalimu Nyerere (NRC) lilianzishwa mwaka 2014 kama mradi huru uliokuwa chini ya Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH). Malengo ya NRC yalikuwa ni kutengeneza makavazi yatakayo tumika kwa ajili ya kutunzia nyaraka na machapisho mbalimbali yaliyokuwa yanapatikana wakati wa utekelezaji wa mradi wa uandishi wa Wasifu wa Mwalimu Nyerere (Mwalimu Nyerere Biography), na pia kuyafanya machapisho hayo yaweze kuwa wazi kwa watafiti na wanazuoni mbalimbali. Vile vile, NRC ilikuwa na lengo la kutoa jukwaa huru la mawazo na fikra za kimkakati kuhusiana na masuala nyeti ya kimaendeleo kupitia mihadhara, semina, mazungumzo, warsha, maonesho, machapisho mbalimbali pamoja na uandaaji wa kozi fupifupi katika nadharia za mifumo na methodolojia za utafiti na maendeleo.

Katika miaka yote mitano ya uhai wake (2014 – 2019), mradi wa Kavazi la Mwalimu Nyerere ulifanya na kufanikisha mambo mengi sana kupitia shughuli zake. Baadhi ya shughuli kuu na ambazo zilikuwa na mguso sana kwa washiriki na umma kwa ujumla zilikuwa ni pamoja na Mihadhara ya Mwalimu Nyerere (Nyerere Dialogue Lectures). Mihadhara hii ilikuwa ikiandaliwa na NRC na kutolewa na wahadhiri mbalimbali wa ndani na nje ya nchi waliokuwa wakialikwa na Kavazi. Kwa ujumla, mihadhara sita iliandaliwa katika kipindi cha miaka hiyo mitano, na kuhudhuriwa na maelfu ya washiriki kutoka pande mbalimbali za nchi pamoja na kurushwa moja kwa moja au kuripotiwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari nchini. Mada tofauti tofauti zilikuwa zikiwasilishwa na kujadiliwa na washiriki wote, baadhi yake zikiwa ni mada kuhusu Nyerere na Umajumui wa Afrika; Elimu ya Juu na Maendeleo ya Afrika; Ubepari, Ujamaa na mifumo ya uzalishaji mali; Jinsia n.k.

Vile vile, pamoja na mihadhara hiyo, Kavazi la Mwalimu lilikuwa linaandaa mijadala na mazungumzo mengine mbalimbali ya wazi kuhusiana na masuala anuai yenye mguso kwa jamii na taifa kwa ujumla, hususan kwa kuzingatia mitazamo na falsafa za Mwalimu Nyerere. Mijadala hii ililenga kuchokonoa na kuibua hoja mbalimbali kutoka kwa washiriki kwa dhumuni la kujenga uelewa zaidi wa masuala husika pamoja na kuwawezesha washiriki kutoa maoni yao kwa kuyaelekeza kwa walengwa mbalimbali wakiwemo watawala, wasomi na wataalamu na umma kwa ujumla. Shughuli nyingine kuu za Kavazi la Mwalimu katika kipindi hicho zilikuwa ni kuandaa na kuchapisha nyaraka, vitabu na machapisho mengine mbalimbali; kuendesha semina fupifupi za mafunzo yenye kuwalenga wataalamu na wanazuoni mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi na kuandaa maonesho ya picha na nyaraka adimu kuhusiana na maisha na falsafa za Mwalimu Nyerere lakini pia kuhusiana na masuala mengine mengi mtambuka yenye kuigusa na kuiathiri jamii na taifa kwa jinsi na namna mbalimbali.

Kwa ujumla, Kavazi la Mwalimu lilifanikiwa kwa kiasi kikubwa sana katika kutengeneza jukwaa lililoweza kuwaleta pamoja wanazuoni, wanasiasa, wataalamu, wasanii, viongozi wastaafu wa kitaifa, wakulima na wafanyakazi na umma kwa ujumla kuweza kusikiliza hoja mbalimbali na kushiriki. Zaidi ya hapo, hayo yote yaliweza kufanyika na kufanikiwa pasipo ubaguzi wa namna yoyote ile kwa washirika kama ubaguzi wa kitabaka, kielimu, kisiasa, kiuchumi, kiumri au hata rangi.

Ukubwa wa mguso wa shughuli za Kavazi katika miaka yote hiyo mitano haukuwa tu kwa maelfu ya washiriki waliokuwa wakihudhuria moja kwa moja matukio hayo, bali pia hadi kwa vyombo mbalimbali vya habari nchini ambavyo navyo havikubaki nyuma katika kurusha matangazo ya matukio hayo moja kwa moja au kwa kuyatolea taarifa zake kwa namna mbalimbali na kuzisambaza kwa umma.

Maudhui ya Kavazi pia yalijikita sana katika kuangazia masuala ya kiaidiolojia tangu enzi za Mwalimu Nyerere hadi sasa. Mijadala na mihadhara mingi iliyofanyika ilitumika kama njia ya kuwawezesha na kuwaongoza washiriki kutafakari, miongoni mwa mambo mengine, mwelekeo wa kitaifa kiaidiolojia na kimaadili. Katika mijadala, washiriki wakijikita katika kujaribu kupata majibu na uelewa wa pamoja na pale iliposhindikana waliielekeza Kavazi kutafuta namna ya kuwawezesha wanakavazi na watanzania kwa ujumla kuchimbua zaidi kiudadisi.

Kama ilivyoelezewa hapo juu, mradi huu wa Kavazi la Mwalimu Nyerere (NRC) ulifungwa rasmi Disemba 31, 2019 na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH). Hata hivyo, taarifa zake nyingi na zilizotokana na shughuli zake na machapisho yake yaliyoandaliwa katika kipindi hicho sasa vinaweza kupatikana katika tovuti ya mahsusi RLS ambayo ni https://ols.rosalux.or.tz/en.

Close